Rais Kikwete akiri kupata wakati mgumu baada ya kuuona mwili wa Marehemu Mzee Mandela. | MIKENTOBI MIKENTOBI - A Blog with updated posts about events and current issues!
NEWS UPDATE :
Over a 100,000 ways to Earn Online!Sale Online!
Labels :
Home » , » Rais Kikwete akiri kupata wakati mgumu baada ya kuuona mwili wa Marehemu Mzee Mandela.

Rais Kikwete akiri kupata wakati mgumu baada ya kuuona mwili wa Marehemu Mzee Mandela.

Written By Mike Ntobi on Saturday, December 14, 2013 | 8:51 AM


Rais Jakaya Kikwete amesema amepata wakati mgumu alipouona mwili wa Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, alipokwenda kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo.

Rais Kikwete alikuwa miongoni wa marais na wageni wengine mashuhuri waliopewa nafasi za kwanza kutoa heshima za mwisho kwa Mandela, juzi katika Ikulu ya Pretoria ambayo iko katika Majengo ya Umoja (Union Buildings).

"Ni vigumu kufikiria kwamba nilichokiona ni kweli….kumwona Mzee Mandela akiwa amelazwa katika jeneza ni ngumu sana kuamini, nimepata wakati mgumu sana," alisema Kikwete.

Rais Kikwete alisema kwa kusitasita huku akionekana mwenye sura ya huzuni.
Rais alikuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Afrika Kusini (SABC) baada ya kutoa heshima za mwisho kwa Mandela.

Kikwete ambaye pia aliungana na viongozi wengine katika ibada ya kitaifa katika Uwanja wa FNB, Jumanne, aliondoka kurejea Tanzania juzi baada ya kutoa heshima za mwisho.
Kwa upande wake Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe alisema Mandela alikuwa mwanamapinduzi mwenzake na kifo chake ni pigo kubwa kwa wanamapinduzi wa Afrika.

"Tulisafiri katika barabara moja, tulibeba mizigo inayofanana; ambayo ni kuumizwa na kuongoza watu wetu, yeye kwangu alikuwa kaka na mkubwa wa umri, tumempoteza na tutamkumbuka,alisema Mugabe.

Viongozi wengine wa Afrika ambao walihojiwa na SABC walimzungumzia Mandela kama mwalimu aliyewafunza somo la uongozi ambalo hawapaswi kuliacha kwa ajili ya wananchi wao na Bara la Afrika kwa jumla.

Rais wa Malawi, Joyce Banda yeye alisema: "Ni mwalimu ambaye alitufunza somo la uongozi, tunapaswa kuhakikisha kwamba tunalizingatia kwa ajili ya kuwaendeleza watu wetu ambao wanakabiliwa na matatizo mengi."

Aliongeza: "Mandela alipigania elimu na hili ni jambo muhimu kwa nchi zetu na vizazi vya sasa, tunapaswa kuyapa kipaumbele mambo haya na mengine mema aliyotufunza".

Rais Mstaafu wa Ghana, Jerry Rawlings alisema Mandela alikuwa na mamlaka ya mambo yote aliyokuwa akiyazungumza na kuwaasa Waafrika na dunia kwa kuwa alikuwa ni mtu wa vitendo.

"Alikuwa mtu mwenye sifa hizo na hakuwa mmoja wetu ambaye angempa changamoto kwamba anasema asichotenda, huu ni mfano ambao sisi viongozi wa sasa tunapaswa kuufuata," alisema Rawlings.
Share this article :

Related Posts :

Post a Comment

 
Support : MIKENTOBI | Creating Website | Johny Template | Mas Template | UviOo | SFI

Copyright © 2010 - 2014. MIKENTOBI - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Modified and Published by MIKENTOBI
Proudly powered by Blogger