Magazeti ya Marekani yameripoti kuwa shambulizi lililofanyika nchini Kenya kwenye jumba la Westgate Naiorbi lilifanywa na watu wasiozidi wanne tu ambapo ripoti hiyo iliyofanyiwa uchunguzi na kitengo cha polisi cha jiji la New York, inapingana na ripoti zilizotolewa na idara za ulinzi nchini Kenya ambazo zilisema shambulizi hilo lilifanywa na watu zaidi ya 15 wakiwemo raia wa nje.
Zaidi ya watu 60 pamoja na wanajeshi sita walipoteza maisha kwenye shambulizi hilo Septemba 21 na magaidi wa kikundi cha al shabab kinachoshirikiana na al qaeda ambapo baada ya kulizunguka jengo la Westgate kwa siku mbili, mamlaka za usalama za Kenya zilithibititsha taarifa kuwa zimerejesha hali ya usalama huku magaidi wanne wakiwa wameuwawa.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne asubuhi, kamishna wa polisi wa New York Ray Kelly amesema wapelelezi hawakujua watu wangapi walihusika na shambulio hilo lakini waliamini kuwa walikuwa watu wanne.
Ripoti hiyo ya NYPD ilisema washambuliaji walibeba silaha nyepesi na hakukuwa na ushahidi unaoonyesha kuwa magaidi hao walijaribu kushika watu mateka baada ya saa 12 na dakika 15 septemba 22.
Ripoti hiyo pia inasema kuwa gaidi kutoka Uingereza ambaye anafahamika kwa jina la White Widow hakuhusika moja kwa moja na tukio hilo japo taarifa nyingi zilionyesha kwamba alihusika na alikuwemo ndani ya Westgate siku ya tukio.
Ripoti nyingine inasema kuwa wanajeshi wa Kenya waliiba vitu kwenye maduka ya westgate na mmoja wa viongozi wa idara ya polisi ya New York mpelelezi Kevin Yorke ambaye aliaandaa na kuwasilisha ripoti hiyo, alikanusha taarifa zilizothibitishwa na Wakenya kuwa magaidi wote walifariki dunia baada ya milipuko kutokea.
Ripoti hiyo inasema kuwa magaidi wanne waliogawanyika kwenye timu mbili za watu wawili waliendesha shambulizi hilo huku wakiwasiliana kwa simu za mkononi na uwezekano upo kabisa kwamba wote walitoroka wakiwa hai.