12/26/12 | MIKENTOBI MIKENTOBI - A Blog with updated posts about events and current issues!
NEWS UPDATE :
Over a 100,000 ways to Earn Online!Sale Online!
[ New Posts ] : Habari Mpya Zote - HAPA CHINI!!!
Labels :

JK:Achangia Milioni 30 Mradi Wa Kuhifadhi Mbwa Mwitu

Written By Mike Ntobi on Wednesday, December 26, 2012 | 10:13 AM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametoa shilingi milioni 30 kuchangia mradi endelevu wa kulea na kuhifadhi mbwa mwitu waliokuwa wameanza kutoweka kabisa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
Mhe. Rais pia amezishukuru na kuzipongeza taasisi za umma na binafsi zinazoshiriki katika kuufanikisha mradi huo unaojulikana kama Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs Conservation Project. 

"Juhudi hizi za kurudisha tena makundi ya mbwa mwitu kwenye mbuga hii inayojulikana  kimataifa ni ya kupongezwa kwani itahakikisha kwamba wanyama hawa wanaendelea kuwepo Serengeti na pia itaongeza idadi ya  vivutio vyetu vya utalii mbugani humu", alisema Mhe. Rais 


Aliyasema hayo  Jumapili Desemba 23, 2012 wakati wa sherehe za  kuachiwa huru kundi la pili lenye mbwa mwitu 15 waliokuwa wamehifadhiwa kwa miezi kadhaa kwenye boma maalumu la mradi huo,  lililojengwa katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara. 
H.E. Dr. J.M. Kikwete
Pres of Tanzania
"Nashukuru taasisi zote zinazounga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha kwamba mbwa mwitu wanakuwepo kwa wingi mbugani  Serengeti kama ilivyo katika mbuga zingine", aliongezea Mhe. Rais.


Katika taarifa yake wakati wa sherehe hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk. Simon Mduma, alimueleza Rais Kikwete kuwa jumla ya Mbwa mwitu ishirini na sita (26), wamerudishwa mbugani hadi sasa, kufuatia  kundi la kwanza la wanyama mwitu hao kumi na moja (11) kuachiwa siku ya Alhamisi Agosti 30, 2012. 


Alitanabahisha kwamba  mradi huo unaohusisha  mbwa mwitu walioondolewa katika msitu wa Samunge wilayani Loliondo ni mojawapo ya juhudi za kurudisha tena makundi ya wanyama hao katika mbuga hiyo maarufu duniani, na kwamba baada ya kuhifadhiwa na hatimaye kuachiwa kwao huku wakiwa wamevishwa collar  maalumu zenye redio ili kufuatilia nyendo zao,  ni muendelezo wa juhudi za kupata makundi sita yenye mbwa mwitu takriban kumi (10) kila moja, ikiwa ni hatua endelevu ya muda mrefu ya kuhakikisha  uwepo wa wanyama hao mbugani humo.  


Dkt. Mduma alisema  kundi la kwanza la mbwa mwitu hao kumi na moja (11) wote wapo hai na wanaendelea vizuri katika maisha yao mbugani humo, na kwamba pamoja na wanyama hao kutembelea hadi maskani yao ya awali ya Loliondo, malalamiko ya kuwapo kwa uharibifu wa mifugo sehemu hizo kama ilivyokuwa awali hayajaripotiwa hadi sasa.


Mkurugenzi Mkuu huyo wa utafiti wa wanyama pori alieleza kuwa mbwa mwitu wamekuwa wakitoweka kutokana na kuuawa kwa sumu na wananchi baada ya kula mifugo yao, ama kwa  kuugua  magonjwa mbalimbali kama vile kichaa cha mbwa.


"Hivi sasa kuna makundi 11 yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu katika Hifadhi ya Ngorongoro, yakifanya idadi ya mbwa mwitu kuwa 200", alisema Dkt Mduma.


Aliongezea kuwa awali, katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti makundi ya mbwa mwitu yalikuwa yakionekana kwa wingi, lakini yamekuwa yakitoweka kwa kasi sana kiasi hata mara ya mwisho ni wanyama mwitu hao  wawili tu walioonekana katika mbuga ya Serengeti mnamo mwaka 1998.  


Mbwa mwitu ni miongoni mwa wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka duniani. 


Takwimu zinaonyesha kuwa  katika Bara la Afrika kuna mbwa mwitu takriban 8,000 na kwamba Tanzania pekee inakadiriwa kuwa  na wanyama hao 3,500 katika mbuga mbalimbali nchini, isipokuwa katika Hifadhi h ya  Taifa ya Serengeti ambako walianza kutoweka  kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha kuanza.  


Kampuni  ya simu za mkononi ya Vodacom imechangia  dola za Marekani 450,000 kwa kipindi cha miaka mitatu ili kufanikisha mradi huo, ambao ulizinduliwa rasmi mwezi Julai mwaka 2011. 


"Vodacom tunajisikia furaha sana kuwa sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya utalii  ambayo kwa sasa mchango wake ni mkubwa sana kwa taifa", alisema Bw. Salum Mwalimu, Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom wakati wa sherehe za kuwarudisha mbugani mbwa mwitu hao 15.


Bw. Mwalimu alisema kampuni yake siku zote inalenga kubadili maisha ya watu na kwamba ni wazi kuimarika kwa Hifadhi  ya Taifa ya Serengeti inayochangia kwa kiasi kikubwa  sekta ya utalii nchini na ambayo inategemewa kwenye kuongeza pato la Taifa na ustawi wa watu ni jambo muhimu sana.

Mwisho.
Taasisi zingine zinazoshiriki katika  zoezi hilo  ni Idara ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya  Ngorongoro (NCCA),  Frankfurt Zoological Society (FZS) , Grumeti Fund (GF) na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. 


Imetolewa na:


Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Desemba, 2012

Meya Jerry Slaa Ashiriki Kampeni Ya Usafi Gongo La Mboto


Pichani Juu na Chini ni Mstahiki Meya wa Ilala na Diwani wa Kata ya Gongo la mboto, Jerry Silaa akiwa na baadhi ya wakazi wa Kata hiyo wakifanya kazi ya usafi katika eneo la Stendi ya Mabasi ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhimiza usafi na kuhifadhi mazingira katika jiji la Dar es Salaam iliyozinduliwa na makamu wa Rais mwanzoni mwa mwezi huu. 



Mstahiki Meya wa Ilala na Diwani wa Kata ya Gongo la mboto,Jerry Silaa akizungumza na baadhi ya wakazi wa Kata hiyo wakati wa kufanya usafi katika eneo la Stendi ya Mabasi ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhimiza usafi na kuhifadhi mazingira katika jiji la Dar es Salaam iliyozinduliwa na makamu wa Rais mwanzoni mwa mwezi huu. 

CCM UK Watoa Salamu Za Heri Ya Krismass


Simba Yashika Nafasi Ya Tatu (3rd) Kombe La Uhai


Release No. 201
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 23, 2012

SIMBA YAPATA NAFASI YA TATU KOMBE LA UHAI

Simba imetwaa nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu zenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuitandika Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 3-0.

Hadi mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam, Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.

Mabao yote ya washindi katika mechi hiyo yalifungwa na Ramadhan Mkipalamoto. Mfungaji alifunga bao la kwanza dakika ya 43 wakati mengine alipachika dakika za 57 na 70. Kwa kunyakua nafasi ya tatu, Simba imeondoka na kitita cha sh. 500,000.

Mechi ya fainali ya michuano hiyo kati ya Azam ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga itachezwa leo (Desemba 23 mwaka huu)  saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Mbali ya kombe, bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai atapata sh. milioni 1.5 wakati makamu bingwa atazawadiwa sh. milioni 1.

Timu iliyoonesha zaidi mchezo wa kiungwana (fair play) itapata sh. 400,000, mchezaji bora wa mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh. 300,000 na kipa bora sh. 300,000. Naye kocha bora katika mashindano hayo atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa bora.

RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI MUSA RICO

Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Coastal Union, Musa Rico kilichotokea jana (Desemba  22 mwaka huu) jijini Tanga.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti akiwa mchezaji Rico, na baadaye kocha alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha ikiwemo Coastal Union, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Rico, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko yanatarajiwa kufanyika leo (Desemba 23 mwaka huu) mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Rico mahali pema peponi. Amina

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TAREFA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 22 mwaka huu).

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Tabora.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAREFA chini ya uenyekiti wa Yusuf Kitumbo aliyeshinda kwa kura 16 dhidi ya nane za Musa Ntimizi, na Paul Werema ambaye hakupata kura.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Tabora kwa kuzingatia katiba ya TAREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti), Fate Remtulla (Katibu), Dick Mlimuka (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Razak Irumba (Mwakilishi wa Klabu TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Eric Kabepele na Mwalimu Sizya.

TWFA YAWATUZA TENGA, FURAHA FRANCIS

Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania (TWFA) kimetoa tuzo kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na Meneja wa timu ya Taifa (Twiga Stars), Furaha Francis kutokana na mchango wao katika kuendeleza mchezo huo.

Tuzo hizo zilitolewa katika Mkutano wa Uchaguzi wa TWFA uliofanyika Desemba 19 mwaka huu mjini Morogoro kutokana na mchango wao katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake nchini.

“Ni dhahiri kazi ya kuendeleza soka ya wanawake ni wajibu wa Shirikisho (TFF), lakini Rais wa TFF alitoa kipaumbele zaidi na alijitoa kuhakikisha misingi imara ya kuendeleza soka ya wanawake inawekwa,” alisema Mwenyekiti wa TWFA, Lina Kessy.

Pia Mkutano huo ulitambua na kumpa tuzo Furaha Francis ambaye amekuwa Meneja wa Twiga Stars kwa miaka minane mfululizo. Licha ya kuwa Meneja wa Twiga Stars, ametumia muda wake na kujitoa katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake.

TWFA itaendelea kutumia michango yao katika mpira wa miguu kwa wanawake nchini.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Njombe, Iringa Waponda Matokeo Darasa La Saba


Na: Shaban Lupimo, Njombe
WANASIASA wa Mikoa ya Iringa na Njombe  wameponda matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa  na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa, kwa kusema kuwa Serikali inapika bomu la wasomi ambao hawatakuwa na tija kwa  taifa.


Wanasiasa hao walitoa kauli hiyo juzi  katika mkutano wa kuchagua wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza katika muhula ujao wa masomo wa mwaka 2013 kwa kanda ya Iringa, uliofanyika mjini Njombe ambapo walielezewa kushangazwa kwao na Serikali kuchagua hata wanafunzi wenye ufaulu D kwenda sekondari.

Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema elimu ya Tanzania imekosa mwelekeo kutokana na mwaka huu Wizara ya Elimu kuchagua wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mpaka waliopata wastani wa alama ya asilimia 24 kwa kila somo, badala ya asilimia 44 ili kujaza nafasi katika shule za sekondari.

“Serikali inapika bomu la wasomi ambao hawatakuwa na manufaa kwa taifa, kwa sababu haiwezekani kuchagua mpaka mwanafunzi asiyekuwa na sifa ya kujiunga na kidato cha kwanza ili kujaza nafasi, wasomi hawa ndio wale wanaopasua watu vichwa badala ya miguu,” alisema Msigwa.

Mchungaji Msigwa aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuacha kujitapa kwamba mwaka huu wanafunzi wamefanya vizuri ikilinganishwa na mwaka jana, wakati wamechukua mpaka wale waliofeli kujiunga na elimu ya sekondari na kuitaka Wizara ya  elimu na mafunzo ya Ufundi kueleza sababu ya  kushusha alama za ufaulu kwa  wanafunzi mwaka huu. 

NayeMbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikujombe (CCM) alisema haina maana kuona taifa linapeleka wanafunzi wengi sekondari wakati waliofaulu ni wachache.

“Mimi naona haina maana kujisifia kuwa tumefaulisha na kupeleka sekondari wanafunzi wengi wakati waliofaulu wachache, kama wamefaulu wanafunzi 100 tupeleke hao hao badala ya 200 ili kujaza shule,” alisema Filikujombe.

Filikunjombe alipendekeza wanafunzi ambao  wamepata wastani wa alama ya chini ya asilimia 70 kuachwa kabisa kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari,  badala ya kuwapeleka sekondari ili kwenda kujaza  vyumba vya madarasa wakati hawana sifa ya kujiunga na elimu hiyo.

Lema Kuzoa Sh85 Milioni


 Na :James Magai na Musa Juma

MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema, huenda akazoa kitita cha Sh85 milioni ambazo ni malimbikizo ya mishahara na posho mbalimbali ambazo hakulipwa wakati alipokuwa nje ya Bunge.


Lema amekuwa nje ya Bunge kwa miezi minane, kuanzia Aprili 5 mwaka huu wakati alipovuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, hadi aliporejeshewa ubunge wake Ijumaa wiki iliyopita na Mahakama ya Rufani ambayo ilikubali rufaa yake iliyopinga uamuzi huo.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah jana alisema baada ya kurejea bungeni, Lema atalipwa stahili zake zote anazostahili kwa muda wote wa siku 260 ambao alikwa nje ya Bunge.

Ingawa ofisi hiyo ya bunge haikusema atalipwa shilingi ngapi, uchambuzi wa malipo na stahili za wabunge umebaini kuwa mbunge huyo kupitia Chadema, atalipwa kitita cha Sh85 milioni ikiwa ni mshahara wake na posho kwa kipindi cha miezi nane alichokuwa nje ya Bunge.

Hata hivyo, Lema mwenyewe aliliambia gazeti hili jana kuwa, malipo yake yanaweza kufikia Sh60 milioni.

Lema aliyeibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, April 5, 2012, kufuatia kesi iliyofunguliwa na makanda watatu wa CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel, wakipinga ushindi wake.  Hata hivyo, Desemba 21,2012, Mahakama ya Rufani ilimrejesha bungeni, baada ya kushinda rufaa yake aliyokata mahakamani hapo kupinga hukumu na tuzo ya Mahakama Kuu Arusha iliyomvua wadhifa huo.

Tangu alipovuliwa ubunge hadi Mahakama ya Rufani ilipomrejesha tena bungeni, Lema alikuwa amekosa mikutano mitatu ya Bunge yenye jumla ya vikao 84.
Mikutano hiyo ni ule wa mwezi Aprili, mkutano wa Bunge la Bajeti Juni hadi Agosti na mkutano wa Novemba.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Bunge na wakiwamo wabunge wa upinzani na wale wa CCM vilisema kwamba malipo ya mbunge kwa mwezi ni Sh10.7 milioni, yakijumuisha Sh2.3 milioni za mshahara, Sh2.5 milioni za mafuta, posho ya jimbo inayokaribia Sh5 milioni na malipo mengineyo.

Kwa muda wa miezi zaidi ya minane ambao amekuwa nje ya Bunge, malimbikizo ya mshahara wake yanafikia Sh18.4 milioni, posho ya jimbo Sh40 milioni, mafuta Sh20 milioni na posho nyingine Sh6.6 milioni.

Kauli ya Lema
Hata hivyo akizungumza na Mwananchi jana, Lema alisema kuwa ingawa hajui kwa hakika kuwa malipo yake ni kiasi gani, lakini kwa hesabu za haraka, yanafikia Sh60 milioni.
Alisema wakati wa kesi hiyo ikiendelea hakuwahi kuwaza kwamba angerejeshwa bungeni, hivyo hakuwahi atalipwa kiasi gani na Bunge.

“Sijui kwanza nitalipwa nini kwani sikuwahi kukaa na kupiga hesabu za malipo haya, maana  najua ubunge  siyo faraja bali ni kuongoza harakati  za kuwasaidia wananchi kutetea haki zao mbalimbali,” alisema Lema.

Alisema alichokuwa akijua ni kwamba  kama akishinda basi, atarejeshewa gharama za kesi yake na makada wa CCM ambao walimfungulia kesi kwani ni malipo yanayotambulika kisheria.

“Najua lazima hawa makada wa CCM, walipe gharama zangu za kesi.Baada ya wao kushinda kesi Mahakama Kuu, Arusha, waliniletea madai ya kuwalipa Sh139 milioni na sasa mimi nawadai zaidi ya milioni 250,” alisema Lema na kuongeza:


Soma zaidi: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Siasa

JWTZ: Tunamsaka Askari Aliyepiga Picha Na Lema & Nassar





 Na: Raymond Kaminyoge Dar na Joseph Lyimo, Simanjiro 

WAKATI Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likihaha kumtafuta aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiwa amevaa sare za jeshi hilo, mtu huyo ameibuka na kusema yuko tayari kufukuzwa kazi kuliko kuacha kuishabikia Chadema.

Kauli hiyo ya JWTZ imekuja baada ya jana, gazeti hili kuchapisha picha ya mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa JWTZ akiwa amepiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, huku akiwa amenyoosha vidole viwili alama inayotumiwa na Chadema.
Baada ya taarifa hiyo, JWTZ lilitoa taarifa likieleza kushtushwa na tukio hilo na kusema kwamba linamtafuta mtu huyo kwa udi na uvumba ili kujiridhisha kama kweli ni askari wake.

‘‘Kimsingi Jeshi linafanya uchunguzi wa kumtambua mtu huyo kama kweli ni askari,’’ ilisema sehemu ya taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo ambayo iliyatilia shaka mavazi aliyokuwa amevaa mtu huyo kama ndiyo yanayotumiwa na jeshi hilo sasa.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema ingekuwa rahisi kumtambua mtu huyo kwa kuangalia paji la uso lakini alilifunika ili asitambulike.
‘‘Pamoja na hayo, jeshi linamtafuta ili kumchukulia hatua za kinidhamu kutokana Kanuni za Majeshi ya Ulinzi likisema Sheria namba Nne ya Mabadiliko ya Nane katika Katiba ya Nchi ya mwaka 1992, Ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa,’’ ilisema taarifa hiyo.

Mbali ya taarifa hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema endapo itabainika kuwa aliyevaa sare hizo ni mwanajeshi, moja ya hatua dhidi yake ni kufukuzwa kazi mara moja.
Mbali na hatua hiyo, Kanali Mgawe alisema kuanzia sasa, Jeshi limepiga marufuku mtu yeyote kuvaa sare zake katika mikutano yote ya siasa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Kuhusu kitendo cha askari huyo kupiga picha na Lema, Kanali Mgawe alisema moja ya masharti muhimu ya askari anapiojiunga na jeshi ni kutambua na kutii sheria inayomzuia kujihusisha na masuala ya siasa na kwamba kitendo cha mtu huyo kimemshangaza na kumfanya amtilie shaka kama kweli ni askari aliyekamilika.

Msimamo wa mtuhumiwa

Kwa upande wake, mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa Kikosi cha Chuo cha Mafunzo Monduli (TMA), mkoani Arusha, alisema ni bora afukuzwe kazi kuliko kunyimwa kujiunga na Chadema.
Akizungumza jana kwa sharti la kutotajwa jina akiwa Mirerani, Simanjiro mtu huyo alisema Chadema ni chama makini chenye uwezo wa kuongoza nchi kwani kinatetea wanyonge na kujali masilahi ya jamii.

Mh.Lowassa Asali Krismas Zanzibar


Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Monduli, Mh. Edward Lowassa akitoa salaam za Xmas kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mwanakwerekwe Zanzibar mara baada ya ibada ya Sikukuu hiyo jana.  Mh. Lowassa, yuko visiwani humo kwa mapumziko ya sikukuu hiyo,ambapo amewataka watanzania kusherehekea sikukuu hizi za krismas na mwaka mpya kwa amani na upendo huku tukilinda umoja na mshikamano uliojengwa na waasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume.


Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Monduli, Mh. Edward Lowassa na mkewe Mama Regina Lowassa wakiungana na Wakristo wengine kwenye ibada ya Sikukuu ya Krismas iliyofanyika jana kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mwanakwerekwe Zanzibar.

Hilall Na Martin Kuwa Waamuzi Unique Model 2012


Baraza la sanaa la aifa limeteuwa majina matatu kati ya sita ya majaji yaliopendekezwa na waandaji wa shindano la kumsaka mwanamitindo wa mwaka mwenye sifa za kipekee. Uteuzi huo wa wabunfu Asia Idarous khamsini, Gymkhana Hilall (paka wear) na Martin Kadinda umefanyika mwishoni mwa wiki hii baada ya baraza la sanaa la Taifa (Basata) kupitia wasifu wao na kuridhika wawe waamuzi rasmi wa shindano la Unique model 2012. 

Kinyang’anyiro cha kumsaka mwanamitindo huyo wa mwaka kinajumuisha washiriki kumi na mbili katika jukwaa moja ambapo fainali hizi zitafanyika tarehe 28 desemba katika ukumbi wa maraha New Maisha club ulioko Oysterbay jijini Dar. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mratibu wa shindano hilo Methuselah Magese amesema kuwa maandalizi ya shindano hilo yako vizuri sana na washiriki wamenorewa kiasi cha kutosha imebaki ni kazi ya umatiwa wapenzi wa mambo ya mitindo kujitokeza kwa wingi kushuhudia nani atachukua taji siku ya ijumaa. 

Shindano la unique model litapambwa na burudani toka bendi ya mashujaa ikiongozwa na rapa maarufu Chalz Baba ikiambatana na ngoma za asili toka kwa Costa Siboka na utambulisho wa msanii mkali wa bongo flava B-shop kwa mara kwanza atatoa burudani ambayo haijawahi kutokea. Magese aliongeza kuwa mbali ya burudani kutakuwa na zulia jekundu(Red carpet) kwa watu maarufu na watu waliopendeza zaidi siku hiyo ambapo kiingilio kitakuwa ni Tshs 15,000 tu kiingilio ambacho hakitengi tabaka la watu flani katika jamii.

Maaskofu Watoa Tamko Juu Ya Masuala Mbalimbali


MKUTANO MKUU WA NNE WA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA 
(TANZANIA CHRISTIAN FORUM (TCF)

TAMKO RASMI  

“ATUKUZWE MUNGU JUU MBINGUNI, NA DUNIANI IWE AMANI KWA WATU ALIOWARIDHIA” 

Utangulizi

Katika Mkutano Mkuu wa Nne wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, Tanzania Christian Forum – TCF, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Desemba, 2012; Wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa mahusiano baina ya Dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini Tanzania, pamoja na kutathmini juu ya wajibu wa Kanisa na Utume wake wa Kinabii kwa taifa letu.

Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) linajumuisha taasisi kuu za Umoja wa Makanisa nchini kama ifuatavyo;-
- Jumuiya ya Kikristo Tanzania - CCT
- Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania - TEC
- Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania - PCT
- Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (observers)

Tafakari

Tafakari yetu ilianza kwa kujiuliza yafuatayo:

1. Ni mwenendo gani uliotusibu hivi karibuni kusababisha kukutana kwetu hapa? 
Vikundi vya kihalifu vikiongozwa chini ya mwavuli wa waamini wa Kiislamu vimekuwa vikishambulia kwa ukali na kikatili sana imani, mali, majengo na makanisa ya Wakristo kwa jeuri na kujiamini.

2. Kwa mwenendo huo ni kitu gani kilicho hatarini? 
Vitendo na mienendo yote ya namna hiyo inahujumu sana Amani, Mapatano na Uelewano kati ya watu wote nchini mwetu. Tunaelewa kwamba ni waamini wachache tu wenye kutenda maovu hayo, lakini mienendo ya kikatili ya namna hii huchochea shari miongoni mwa walengwa wa ukatili husika na kutaka kulipiza kisasi hata kusababisha uvunjifu wa amani.

3. Ni athari gani kwa nchi, katika muda ujao, iwapo mienendo hiyo haitadhibitiwa na kukomeshwa kabisa? 

Katika nyakati zetu hizi, tunashuhudia fadhaa na migogoro mingi ya kijamii. Kuna hasira kubwa ya chinichini inayotokana na kasoro nyingi za kiutendaji katika mihimili mikuu ya uongozi na utando mkubwa wa ufukara wa kutupwa kwa wananchi wengi usio na matumaini ya kumalizika hivi karibuni. Hatari ya hali hii ni dhahiri kwamba makundi nyemelezi (kisiasa, kiuchumi na kidini), kwa kutumia vikundi halifu vilivyo katika hali ya ufukara na migogoro, yatavielekeza kimapambano na kiharakati kutetea kijeuri ajenda hasimu za wale walio madarakani au washindani wao kwa maslahi ya wanyemelezi. Hali tunayoelezea sio ya kufikirika kwani ndiyo inayotokea huko nchini Nigeria, Kenya na nchi za Afrika ya Kaskazini hivi sasa. Tanzania haina kinga ya kipekee kuiepusha kukumbwa na maovu ya namna hiyo bila utaratibu na vyombo thabiti kuhimili mienendo hasi kama hii. Kutokana na matukio na kauli zinazotolewa na watu mbalimbali hapa nchini, inawezekana tayari wanyemelezi wako kazini wakiongoza vikundi kusukuma ajenda za kutekeleza maslahi yao.

4. Masuala yanayotakiwa kufafanuliwa na kudhibitiwa na Dola mapema ili yasiendelee kupotoshwa:
  • Hali ya mahusiano kuzorota pamoja na kashfa dhidi ya Kanisa.

Huu ni wakati wa kukubali kwamba misingi ya Haki, Amani na Upendo katika Taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa. Uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa wazi na makusudi unaofanywa na baadhi ya waamini wa dini ya Kiislamu, ukiendeshwa na kuenezwa kupitia vyombo vyao vya habari vya kidini (redio na magazeti) mihadhara, kanda za video, CD, DVD, vipeperushi, makongamano, machapisho mbalimbali na kauli za wazi za viongozi wa siasa na hata viongozi wa dini husika (ushahidi wa mambo yote haya tunao) pasipo Serikali kuchukua hatua yeyote huku bali imekuwa ikibakia kimya tu. Ukimya huu unatoa taswira ya Serikali kuunga mkono chokochoko hizi. Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivi hivi linaashiria hatari kubwa ya kimahusiano siku zijazo.
  • Hadhi ya Baba wa Taifa kuhifadhiwa.

Huyu ni kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu akitetea Watanzania wote bila ubaguzi wowote, akiimarisha umoja wa Kitaifa, amani na upendo kwa watu wote. Kashfa, kejeli na habari za uongo dhidi yake ni kukipotosha kizazi hiki na hata vizazi vijavyo kwa kuondoa moja ya alama muhimu ambazo kiongozi huyo alisimamia kwa ajili ya umoja wa kitaifa.
  • Memorandum of Understanding” (M.o.U) ya mwaka 1992, kwa ajili ya huduma za kijamii zitolewazo na Makanisa kwa Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na huduma za hospitali, vituo vya afya na zahanati na shule mbalimbali zinazoendeshwa na Makanisa nchini kote. Ni vema ikaeleweka wazi kwamba makubaliano hayo (M.o.U) yalikuwa ni kati ya Makanisa ya Tanzania na Makanisa ya nchini Ujerumani ambapo Serikali ya Tanzania ilihusishwa tu, kwa vile raia wake ndio wangenufaika na misaada hiyo ambayo nchi ya Ujerumani ingeitoa kupitia Makanisa hayo. Kanisa limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru na baada ya uhuru pasipo ubaguzi. Ikibidi ni vema kuondoa hali hii, ya Kanisa kuendelea kutukanwa, chuki na kukashifiwa viongozi wake kutokana na huduma hizi kwa jamii yote. Jukwaa la Wakristo Tanzania tunaitaka Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya M.o.U hiyo, maana yake, makusudi yake na manufaa yake kwa Watanzania wote.

  • Hujuma ya kuchomwa Makanisa na mali za Kanisa, ni tukio la uvamizi na uchokozi wa wazi, ulioyakuta makanisa yetu na waamini wake wakiwa hawana habari na bila maandalizi yoyote. Ni muhimu kuanzia sasa, Wakristo wote wakae macho na wawe waangalifu zaidi.

  • Dhana ya kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo Kristo ni potofu na potevu.

Maneno hayo ni ushahidi wa uwepo wa ajenda za waamini wenye imani kali na waliojiandaa kwa mapambano maovu kutetea dhana potovu kinzani na misingi ya demokrasia na haki za binadamu kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa na kuridhiwa na Serikali yetu. Jukwaa la Wakristo nchini tunakanusha wazi wazi na kueleza bayana kuwa, nchi hii haiongozwi kwa mfumo Kristo!. Kwa watu walio makini hakuna kificho kuwa viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu Serikalini awamu ya sasa, asilimia 90 ni Waislamu (Rais wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi). Kwa mantiki hiyo haiingii akilini kueleza watu kuwa nchi hii inaendeshwa kwa mfumo Kristo! Kwa upande wa Zanzibar asilimia 100 ya viongozi ngazi za juu Serikalini ni Waislamu, na sio kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa za kuongoza. Kisha, hata uwakilishi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu. Tunayo mifano mingine mingi iliyo wazi, na hii ni baadhi tu. Watanzania wanapaswa kuelewa wazi kuwa, nchi hii inaongozwa kwa misingi ya Utawala wa Kisheria na sio vinginevyo.
  • Matumizi hasi ya Vyombo vya Habari vya Kidini:

Vyombo vya habari vya kidini vinatumiwa na viongozi wa dini ya Kiislam kuukashifu Ukristo na kuwachochea Waislamu hadharani kupitia vyombo hivyo wakiwataka wawaue Maaskofu na Wachungaji, iwe kwa siri au hadharani. Japo Serikali imesikia kashfa na uchochezi huo hatarishi, imendelea kukaa kimya, na kuwaacha wachochezi hao wakiendelea kuhatarisha amani bila kuwadhibiti. Jambo hili linatia mashaka makubwa juu ya umakini wa Dola kuhusu usalama wa wananchi nchini mwao. Imani kali za namna hii huchochea vitendo viovu vya uasi na hujuma sio tu dhidi ya waamini na viongozi wa dini fulani, bali hata na kwa Serikali na viongozi waliopo madarakani, endapo waamini wa dini fulani katika taifa kama Tanzania lililo na waamini wa dini nyingi tofauti, hawataheshimu na kutendeana kiungwana baina yao na wale wasio wa dini na mapokeo yao. Hali hii inapelekea kujiuliza kama je,huu ni wakati mwafaka kwa kila raia au kiongozi wa dini kujilinda yeye mwenyewe na waamini wake dhidi ya wenye imani kali?
  • Matukio yanayosababisha hasira na kutenda maovu:

Tumejionea matukio kadhaa ambayo kwayo vikundi vya watu wenye hasira vilisababisha hujuma na uharibifu mkubwa wa mali za watu wengine. Hivyo ni viashiria tosha vya uchovu na unyonge mkubwa katika jamii yetu, ambamo jambo dogo tu na hata la kupuuzwa, likitendwa na afikiriwaye kuwa hasimu wa watu fulani, wahalifu hujipatia fursa ya kuonesha hasira yao kwa vitendo vya hujuma na shari, wakiharibu hata kuteketeza mali na nyenzo za maisha ya jamii. Suala hili lataka uchambuzi yakinifu na wa kiroho ili kupata majibu na maelezo sahihi na wala sio kwa kutumia nguvu za ziada za kijeshi au kwa majibu mepesi ya kisiasa. Hili ni suala lihusulo tunu na maadili ya jamii yote ya Watanzania katika ujumla wao. Kila mmoja wetu ni mhusika na sote tukitakiwa kuwajibikiana katika ujenzi wa amani iletayo mapatano na uelewano kati yetu.

Mapendekezo:
Kutokana na muono wetu huo tunapendekeza yafuatayo:
  • Tabia na mienendo ya kukashifiana ikomeshwe kabisa na badala yake tujengeane heshima/staha tukizingatia utu wa kila mmoja katika utofauti wetu.
  • Tumwendee Mungu wetu na kumwomba atuongoze sote kufuata utashi wake tukitafuta huruma yake iliyo sheheni upendo wake mkuu, ili atujalie umoja wa kuishi pamoja kwa amani nchini mwetu.
  • Tunaitaka Serikali yetu na vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kutenda mara moja na bila kuchelewa, katika nyakati ambazo vikundi halifu kisiasa au kidini vinapoanza uchochezi ili kupambanisha wanajamii. Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo hatua mathubuti kuchukuliwa na Dola ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji. Ikithibitika kwamba uharibifu uliofanywa ulitokana na kikundi mahususi chini ya uongozi wa dini au chama cha kisiasa au asasi isiyo ya kiserikali, basi taasisi husika iwajibishwe na kulipa fidia kwa uharibifu uliofanywa.
  • Lianzishwe Baraza mahsusi lililo huru lisiloegemea chama chochote cha kisiasa wala dini yoyote na litamkwe na kuwezeshwa kikatiba likiwa na dhumuni kuu la kuilinda na kuiongoza Serikali kuto fungamana na dini yoyote na kuhakikisha kwamba dira na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye kujali maslahi ya wote havipotoshwi. Baraza hilo liwe na uwezo wa kuvichunguza vyombo vya sheria na usalama itokeapo matatizo makubwa yaashiriayo uvunjifu wa haki na kuteteresha usalama wa nchi.
  • Na sisi viongozi wa dini za Kikristo, Kiislam, Kihindu na nyinginezo tuwajibike katika kufundisha, na katika majiundo ya waamini wetu, hasa vijana, ili kuwajengea uelewa na utashi wa kuvumiliana kwa upendo. Katika kushuhudia na kuadhimisha imani na ibada zetu sote tutambue , tulinde na kukuza maadili, tunu na desturi za imani za watu wengine wanazo ziheshimu na kuzitukuza. Vikundi vya imani kali na pambanishi kwa kutumia kashfa potoshaji sharti vidhibitiwe kwa weledi mkubwa wa viongozi wa dini husika wakisaidiana na usalama wa taifa. Stahamala [kustahimiliana] ni fadhila inayopaswa kufundishwa na kupenyezwa katika mifumo ya uongozi na maisha ya jamii na ihifadhiwe kwa kufuatiliwa kwa karibu sana.


Hitimisho: 
Kwa sasa Kanisa liko katika vita vya Kiroho, hivyo ni vyema Waamini wote wakakumbuka kuwa, katika mapambano kama hayo Mungu mwenyewe, Mwenye enzi yote ndiye mlinzi wa watu wake na Kanisa lake.
JIBU LITAPATIKANA TU, KWA NJIA YA SALA, KUFUNGA NA MAOMBI!

Hivyo siku ya Jumanne tarehe 25 Desemba 2012, inatangazwa rasmi nchini kote kuwa siku ya sala na maombi kwa Wakristo wote na Makanisa yote nchini, pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba kwa imani, amani katika nchi yetu, na kumkabidhi Mungu ashughulikie mipango yoyote iliyopo, ya wazi na ya kisirisiri ya kutaka kuondoa amani ya taifa hili na kuyashambulia Makanisa nchini Tanzania ishindwe na kuangukapamoja na wale wote walio nyuma ya mipango hiyo.

1. Askofu Bruno Ngonyani (TEC) - Mwenyekiti 
2. Askofu Dkt. Israel Mwakyolile (CCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza) 
3. Askofu Daniel Aweti (PCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza) 
4. Askofu Oscar Mnung’a (CCT) - Mjumbe
5. Askofu Elisa Buberwa (CCT) - Mjumbe
6. Askofu Stephen Mang’ana (CCT) - Mjumbe
7. Askofu Dkt. Peter Kitula (CCT) - Mjumbe
8. Askofu Alinikisa Felick Cheyo (CCT) - Mjumbe
9. Askofu Christopher Ndege (CCT) - Mjumbe
10. Askofu Michael Hafidh (CCT) - Mjumbe
11. Askofu Charles Salala (CCT) - Mjumbe
12. Askofu Dismus Mofulu (CCT) - Mjumbe
13. Mchg. Conrad Nguvumali (CCT) - Mjumbe
14. Mchg. Ernest Sumisumi (CCT) - Mjumbe
15. Mchg. William Kopwe (CCT) - Mjumbe
16. Askofu Thaddaeus Ruwa’ichi (TEC) - Mjumbe
17. Askofu Paul Ruzoka (TEC) - Mjumbe
18. Askofu Norbert Mtega (TEC) - Mjumbe
19. Askofu Severine Niwemugizi (TEC) - Mjumbe
20. Askofu Michael Msonganzila (TEC) - Mjumbe
21. Askofu Castorl Msemwa (TEC) - Mjumbe
22. Askofu Eusebius Nzigilwa (TEC) - Mjumbe
23. Askofu Renatus Nkwande (TEC) - Mjumbe
24. Askofu Bruno Ngonyani (TEC) - Mjumbe
25. Fr. Antony Makunde (TEC) - Mjumbe
26. Fr. Sieggried Rusimbya (TEC) - Mjumbe
27. Fr. Ubaldus Kidavuri (TEC) - Mjumbe
28. Askofu Dkt. Paul Shemsanga (PCT) - Mjumbe
29. Askofu Ability Samas Emmanuel (PCT) - Mjumbe
30. Askofu Nkumbu Nazareth Mwalyego (PCT) - Mjumbe
31. Askofu Batholomew Sheggah (PCT) - Mjumbe
32. Askofu Dkt. Mgullu Kilimba (PCT) - Mjumbe
33. Askofu Renatus Tondogosso (PCT) - Mjumbe
34. Askofu Emmanuel Mhina (PCT) - Mjumbe
35. Askofu O.S. Sissy (PCT) - Mjumbe
36. Askofu Jackson Kabuga (PCT) - Mjumbe

Padre Apigwa Risasi Mdomoni Zanzibar


Kwa mujibu wa Breaking News  toka Radio One, Padre anayejulikana kwa jina la Ambrose Mkenda amepigwa Risasi na Watu wasiofahamika kwenye gate la nyumbani kwake wakati akifunguliwa gate aingie nyumbani kwake maeneo ya Kitomondo Mjini Zanzibar, ambako ndiko makazi yake yalipo akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha pekee yake.

Hali yake sio nzuri kwani Risasi aliyopigwa imemdhuru maeneo ya mdomoni. 

Waliompiga Risasi Padre huyo inasemekana ni watu waliokuwa kwenye pikipiki, ambao walimvamia akisubilia afunguliwe gate kuingia nyumbani kwake. 
Get our toolbar!Get our toolbar!
  • Alexaporn - XXX (+18) Search!Alexaporn - XXX (+18) Search!
 
Sell Your Products At TripleClicks!Share Links Earn Money!
cafepress.com/nicemike
Sale Online!
Support : MIKENTOBI | Creating Website | Johny Template | Mas Template | UviOo | SFI

Copyright © 2010 - 2014. MIKENTOBI - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Modified and Published by MIKENTOBI
Proudly powered by Blogger