TAARIFA KWA UMMA
Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania MISA-Tanzania) inasikitika kuarifu umma wa watanzania kwamba inapinga vikali kitendo cha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Magazeti Tanzania Bara kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kuanzia tarehe 30 Julai 2012.
Katika taarifa iliyotolewa na serikali kupitia tangazo lake lililochapishwa kwenye magazeti mbalimbali hapa nchini na kunukuu kutolewa kwa amri hiyo kupitia gazeti la serikali (Government Notice)toleo namba 258 la tarehe 27 Julai 2012, serikali imeeleza kama ifuatavyo:
“Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa mujibu wa sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu namba 25 (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai 2012”
Aidha, tamko hilo la serikali limeeleza pia kuwa sababu za msingi za kulifungia gazeti hilo ni kufuatia machapisho mbalimbali ya gazeti hilo kwenye toleo Na. 302, Na. 303 pamoja na toleo Na. 304 yote yakiwa ya mwezi Julai 2012 pamoja na machapisho mengine yaliyotangulia. Serikali imeeleza kuwa machapisho hayo yamekuwa “yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii”
Hata hivyo, serikali haikubainisha ni habari zipi katika machapisho hayo ambazo zinaeneza na kujenga hofu kwa jamii. Kitendo hicho cha kutobainisha habari husika kinatufanya sisi kama wanahabari na watetezi wa haki ya kupata taarifa pamoja na uhuru wa vyombo vya habari nchini na katika kanda ya kusini mwa Afrika kutoridhia maamuzi ya serikali kwani yamehusisha masuala ambayo hayakuwekwa bayana.
Ni kwa mashaka makubwa ambayo yanatokana na tamko husika la serikali kwa kutumia maneno yafuatayo:
“Kuanzia sasa serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu”
MISA–Tanzania inasikitishwa na kauli hiyo kwani kauli hiyo ni kudhihirisha matumizi mabaya ya sheria zilizopo katika kukandamiza uhuru wa kupata taarifa na uhuru wa vyombo vya habari kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18 (b) na (d) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005.
Haki ya kutafuta, kupata na kutoa taarifa ni haki ya msingi ya kila binadamu na imetambuliwa hivyo na Katiba ya Tanzania. Haki hii imetambuliwa pia na mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia bila masharti yoyote.
Kama kweli kuna taarifa za uchochezi zilizochapishwa na gazeti la MwanaHalisi na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi, ni vyema serikali ingebainisha taarifa hizo kwenye chapisho husika na siyo kuorodhesha machapisho mbalimbali kama sababu yake ya kulifungia gazeti.
Hata hivyo, mamlaka ya serikali kufungia gazeti kupitia msajili wa magazeti ni ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu na matumizi makubwa ya madaraka.
Ni kwa sababu hizo kwamba Ripoti ya Haki za Binadamu iliyowahi kuandaliwa na kutolewa na Tume maalumu iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujulikana kama Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 ilibainisha sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kuwa ni miongoni mwa sheria arobaini ambazo zinakandamiza haki za binadamu nchini. Sheria hiyo haina budi kufutwa kwenye vitabu vya sheria za nchi hii.
Kitendo cha kulifungia gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana kinaweza kusababisha hofu kubwa kwa watetezi wa haki za binadamu na wanahabari kwa ujumla. Kitendo hicho kinafuatia kile cha kuwakamata na kuwaweka rumande (Oysterbay Polisi) wanaharakati zaidi ya kumi kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo kuandamana kufuatia mgomo wa Madaktari mnamo tarehe 9 mwezi Februari 2012.
MISA –Tanzania inalaani vikali matumizi mabaya ya Dola katika kunyamazisha wanahabari wanapojaribu na kuthubutu kufuatilia matukio mbalimbali na kuarifu umma kuhusu yale waliyoyafanyia kazi kwa kina. Ni rai yetu kwa serikali kuwa ni vyema wabainishe taarifa mahsusi zilizopelekea maamuzi ya kufungia gazeti la MwanaHalisi ili kutuondolea hofu sisi tunaotetea haki na uhuru wa vyombo vya habari. Kuendelea kuficha taarifa husika ni kuendelea kuikanyaga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (ibara ya 18) kupitia kivuli cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo kimsingi imepitwa na wakati na haiwezi kutumika kinyume na Katiba ya nchi.
Ni rai yetu pia kwa serikali ya Tanzania kwamba izingatie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika yale yenye kuhamasisha utoaji haki kuliko kujikita kwenye kifungu cha 30 cha Katiba hiyo ambacho kimsingi kinaweka mipaka maalumu ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Mipaka hiyo haionekani kuzingatiwa na serikali katika kulifungia gazeti la MwanaHalisi.
Kwa taarifa hii kwa umma, tunaiomba pia serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulifungulia gazeti la MwanaHalisi mapema iwezekanavyo na bila masharti ili kuwawezesha watanzania kuendelea kunufaika na taarifa zinazochapishwa na gazeti hilo ilmradi maadili ya uandishi wa habari yazingatiwe. Hii ni haki ya msingi kwa kila mtu na ni vyema aione ikitekelezeka.
Taarifa hii imetolewa na kusaini hapa Dar es salaam leo tarehe 31 Julai 2012.
Mohammed Tibanyendera
Mwenyekiti, MISA-TAN
Post a Comment