SASA ni dhahiri kwamba hali si shwari ndani ya Chadema, baada ya viongozi zaidi kuendelea kuachia ngazi kwa kile walichodai kuchoshwa na hali ya mambo katika chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Baada ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi kujiuzulu wadhifa wake mwishoni mwa wiki iliyopita, jana ilikuwa zamu ya Mwenyekiti wa Chadema mkoani Lindi, Ally Chitanda aliyetangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya chama na pia kujivua uanachama.
Mbali ya kuwa Mwenyekiti wa Mkoa, kabla ya uamuzi wake huo uliotangazwa jana, Chitanda pia alikuwa Katibu wa Sekretarieti katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema Taifa katika makao yake makuu yaliyopo Mtaa wa Togo, Kinondoni jijini Dar es Salaam. Alikuwa pia Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa na pia Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Chitanda alianika uamuzi wake huo jana katika mkutano wake na wanahabari mjini Lindi, akisema amechoshwa na unafiki na uonevu unaoendelea ndani ya chama hicho alichojiunga nacho miaka kumi iliyopita akitokea NCCR-Mageuzi.
Alisema kikao cha Kamati Kuu kilichoketi kwa siku mbili na kufikia maazimio kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwavua madaraka Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba ndiyo yaliyomchefua na kuchoshwa na mwenendo ndani ya Chadema.
Akitangaza kujiengua, alisema; "Napenda kuwaambia Wanachadema na Watanzania kwa ujumla, maamuzi haya ya Kamati Kuu ya kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Mkumbo ni maamuzi ya kijuha na yanayowafanya Watanzania sasa waangalie mara mbili mbili kama hawa watu wapo makini na huo ukombozi wanaousema."
Alisema Zitto na wenzake wameonewa, kwani hakuna baya lolote walilolifanya, bali wametoswa kutokana na homa ya uchaguzi mkuu wa ndani ya chama.
"Ni fedheha leo mimi kuwa sehemu ya watu wanaomuita Zitto Kabwe ni msaliti. Siwezi kuendelea na ujinga huu na sipo tayari tena. Si dhambi kumhukumu mtu kwa kuwa anapanga mipango ya kukushinda kwenye uchaguzi, dawa ya mpinzani wako ni kumkabili" Alisema.
Hakuna usaliti, uhaini, Aidha, Chitanda ameeleza kuwa, akiwa mtendaji wa ofisi ya Katibu Mkuu, alishiriki pamoja na Zitto na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa kupanga mikakati mbalimbali, mizuri na mibaya kwa nchi, lakini hawakuwahi kuitwa wasaliti, wahaini wala jina lolote baya.
"Tumekuwa tukiweka mikakati mbalimbali ya ushindi ili chama kishinde, kwa mfano, kabla hata ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (Jeremiah Sumari), wakati tu ilipobainika anaugua, chama kiliandaa mkakati wa kushinda ubunge wa jimbo hilo na uchaguzi uliporudiwa mkakati ule ulitumika na kushinda.
"Naomba nikiri kwamba nikiwa Katibu wa Sekretarieti tumekuwa tukilazimishwa mara kadhaa kuwashawishi wajumbe wengi kutowaunga mkono watu wenye misimamo thabiti ndani ya chama na badala yake tumekuwa tukitumia rasilimali za chama kuwajenga wajumbe 'ndio'," alilalamika Chitanda na kudai kuwa, wakati Dk Slaa akisema mjadala wa Zitto umefungwa rasmi, ni uongo kwa kuwa amewaagiza wakurugenzi wa chama kuzunguka nchi nzima kusambaza waraka waliouandaa ukimchafua Zitto.
Kutokana na mambo yanayoendelea ndani ya chama, amedai nafsi yake haipo tayari kuendelea kuwa sehemu ya upotoshaji dhidi ya Watanzania wenzake.
"Nafsi yangu inanikataza kabisa kuendelea kufumbia macho maovu yanayoendelezwa na chama changu. Nafsi yangu imechoka kuendelea kushuhudia ubaguzi wa kidini na kikabila unaofanywa wazi wazi na viongozi wa chama changu.
"Nafsi yangu imekataa sasa, haipo tayari tena kuwa kuwadi wa kuwahadaa Watanzania kuyafikia matarajio tunayowapa ambayo kamwe hayafikiki. Kwa kuwa siamini kwamba kuvuliwa nyadhifa kwa Zitto Kabwe na Dk Mkumbo ni kwa sababu ya waraka wa ushindi, bali ninaamini kuvuliwa kwao ni kutokana na hofu ya uchaguzi, ubaguzi wa kikabila na kikanda.
"Hivyo basi, nikiwa na akili timamu kabisa, leo tarehe 30.11.2013 nimeamua kujivua nyadhifa zangu zote nilizokuwa nazo ndani ya chama. Sioni tena sababu ya kuendelea kuwa mwanaChadema, sioni tena sababu ya kuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Lindi, sioni tena sababu ya kuwa Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu," alisema.
`Kubebana' katika madaraka.
Licha ya kile alichodai ni uonevu dhidi ya Zitto na wenzake, Chitanda pia alilalamikia upendeleo wa nafasi nyeti ndani ya chama kwamba zimekuwa zikiegemea watu wa upande mmoja.
Mathalani, alisema pamoja na uamuzi wa kuwavua madaraka Zitto na wenzake hivi karibuni, Kamati Kuu pia iliridhia uteuzi wa wakurugenzi watano na kuwaongezea pia maslahi.
Aliwataja wakurugenzi hao ni Benson Kigaila (Mkurugenzi wa Oganaizesheni), John Mnyika (Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano ya Ndani), Anthony Komu (Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji), John Mrema (Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri) na Wilfred Lwakatare (Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama).
Kwa mujibu wa Chitanda, uteuzi huo hauoneshi sura ya kitaifa kwani kati ya kurugenzi zote sita, nne zinaongozwa na watu wanne kutoka Mkoa mmoja wa Kilimanjaro.
Alisema mabadiliko hayo yanakwenda sambamba na posho nono, akisema wakurugenzi waliokuwa wakilipwa Sh 800,000 kwa mwezi, sasa watakuwa wakilipwa kati ya Sh milioni 1.5 na milioni 2.5 wakati maofisa waandamizi waliokuwa wanalipwa Sh 680,000 sasa watalipwa hadi Sh milioni 1.5.
"Pamoja na kwamba uboreshaji uliridhiwa, lakini katika mpango ulioridhiwa na Baraza Kuu ni pamoja na kulipa posho kwa makatibu wa wilaya na mikoa. Hawa ndio watendaji muhimu katika ujenzi na uhai wa taasisi hii lakini, hawakuangaliwa wala kuguswa badala yake wanatakiwa kujitolea tu kwa hali na mali," alisema.
Tangu uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwavua madaraka Zitto na wenzake kwa tuhuma za kupanga mikakati ya `uhaini' ndani ya chama, kumekuwa na mpasuko ndani ya chama, wengine wakiunga mkono uamuzi wa uongozi na wengine wakipinga kwa madai kuwa nguvu kubwa imetumika `kuwaonea' wanasiasa hao vijana, lakini pia wenye nguvu na ushawishi wa kisiasa.
Miongoni mwa wanaotajwa kutoridhika kuondolewa kwa Zitto na wenzake ni mwanazuoni na mkongwe katika duru za kisiasa ambaye pia ni mshauri wa Chadema, Profesa Mwesiga Baregu aliyekaririwa kukionya chama kwa hatua hiyo, akisema haikuwa na ulazima kwa sasa, bali mambo yangeweza kusawazishwa kwa mazungumzo.
Naye Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Temeke na mjumbe wa Baraza Kuu, Patrick Joseph, alitoa kauli iliyodhihirisha kuwa yeye ni mmoja wa wanaomwunga mkono Zitto.
Wengine ni Mwanasheria wa Mbowe, Albert Msando ambaye sasa ni Mwanasheria wa akina Zitto. Wakati Chitanda akiyasema hayo, Ofisa Mwandamizi wa Habari Chadema, Tumaini Makene jana jioni alitoa taarifa inayofafanua madai kadhaa ya Mwenyekiti huyo wa Mkoa wa Lindi aliyejiuzulu.
Katika ufafanuzi wake, alisema hakuna upendeleo katika ugawaji wa madaraka, akisema kati ya wakurugenzi sita waliopo kwa sasa, ni wawili tu ndio wanaotoka Kilimanjaro, Mrema na Komu.
Wengine na mikoa yao ni Mnyika (Mwanza), Kigaila (Dodoma) na Lwakatare (Kagera). Aidha, Makene aliyesema mjadala wa Zitto na wenzake umefungwa na kwamba zinasubiriwa taratibu za kikatiba ndani ya chama, alisema wakurugenzi waliotajwa si wapya katika nafasi zao, bali mpya ni mmoja, ni Mwanasheria Peter Kibatala, atakayesimamia Kurugenzi ya Sheria na Haki za Binadamu. Kibatala ana asili ya Mkoa wa Morogoro.
Amekanusha pia kuwa Chitanda alikuwa Katibu wa Sekretarieti ya Makao Makuu, akisema nafasi hiyo ambayo imo ndani ya Katiba ya Chadema haina mtu mpaka sasa.
"Mahali pengine amejitambulisha kuwa ni Katibu Ofisi ya Katibu Mkuu. Ofisi hiyo ina Katibu Mtendaji mmoja ambaye ni Mzee Victor Kimesera, mmoja wa waasisi wa Chadema," anasema na kuongeza kuwa, kauli ya Chitanda kwamba Zitto na wenzake wameonewa kwa hofu ya uchaguzi inashangaza kwani ni kauli za mara kwa mara zinazotoka kwa mahasimu wa Chadema kisiasa.